DOZI 600,000 ZAPOKELEWA MKOANI GEITA KWA AJILI YA KAMPENI YA SURUA RUBELLA





Na Salum Maige,Geita.

Mkoa wa Geita umepokea dozi  zaidi ya 600,000 za chanjo ya surua rubella kutoka wizara ya afya za kutekeleza  kampeni ya kitaifa ya chanjo ya surua rubella kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa taarifa ya mganga mkuu mkoa wa Geita Dkt Omary Sukari amesema, zoezi la kampeni hiyo limeanza februari 15 hadi 18 mwaka huu na kwamba matarajio ya mkoa huo ni kuwafikia watoto wapatao 517,793.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 mkoa wa Geita unakisiwa kuwa na watoto wapatao 553,228.

Aidha Dkt Sukari amesema, idadi ya dozi zilizopokelewa ni nyingi ukilingaisha na matarajio ya mkoa hivyo, idara ya afya itahakikisha watoto wote wanaotakiwa kupata chanjo wenye umri wa kuanzia miezi tisa hadi miaka mitano wanapata chanjo hiyo.

“Uhamasishaji ni mkubwa mno,kila mahali tumepeleka timu na ukiachilia mbali kutoa huduma hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma, kuna baadhi ya maeneo pia huduma hizo zitatolewa zikiwemo ofisi za serikali za vijiji na mitaa ili kuwasogezea wananchi huduma karibu” anasema Dkt Sukari.

Amefafanua kuwa, lengo la serikali la kuja na kampeni hiyo ni kuwakinga watoto  na maradhi yanayotokana na ugonjwa wa surua rubella unaoadhiri ukuaji wa mtoto.

“Mtoto asipopata chanjo hiyo ana hatari ya kupata udumavu,kupatwa na homa kali,upele na husababisha vifo kwa watoto chini ya miaka mitano,hivyo tunawaomba sana wazazi na walezi kuitikia kampeni hii ili watoto wapate hii chanjo” anasema Dkt Sukari.

Mwandishi wa blog hii amefika katika katika zahanati ya halmashauri ya mji wa Geita na kushuhudia baadhi ya wazazi na walezi wakipeleka watoto wao kupata chanjo.

Wazazi hao ni pamoja na Neema James mkazi wa mtaa wa Mseto na Elizabert Alfredinand mkazi wa mtaa wa Mkoani wamesema, wameitikia wito wa serikali ili kuwakinga watoto wao na hatari ya kupata ugonjwa wa surua rubella.

“Tumehamasika kuja ili kuwapatia haki watoto wetu ya kupata chanjo hii,hivyo hata wazazi wengine walete watoto wao ili kuwakinga na ugonjwa huo surua rubella,na tunaishukuru sana serikali kuleta kampeni hii” wanasema wazazi hao.

Moja ya vikwazo vinavyomwadhiri mtoto katika kufikia hatua sahihi za ukuaji wake ni pamoja na kukosa afya bora hivyo jamii inatakiwa kushiriki kikamilifu wakati wa kampeni hii ili kuwakinga watoto na maradhi yatokanayo na ugonjwa wa surua rubella

Post a Comment

0 Comments