HATIMAYE SERIKALI YAPATA MWAROBAINI WA AJALI KWA WANAFUNZI




Na Salum Maige, Geita.

Hatimaye wananchi kwa kushirikiana na serikali wametatua changamoto ya wanafunzi ya kutembea umbali mrefu na ajali za barabarani wakati wa kwenda na kutoka shule baada ya kukamilisha ujenzi wa shule mpya ya msingi Jineri iliyopo katika kijiji na kata ya Nyamigota halmashauri ya wilaya ya Geita.

Hapa nchini moja ya changamoto zinazowakabili wanafunzi hasa wale wa madarasa ya awali, la kwanza na la pili ambao umri wao ni kati ya miaka mitano hadi nane ni kutembea umbali mrefu na wakati mwingine hukumbana na ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa wakazi wa Mitaa ya Nyamigota, Inyala na Songambele wanasema, katika kipindi cha mwaka 2022/2023 wanafunzi sita walipoteza maisha na 15 kujeruhiwa na wengine kupata ulemavu wa kudumu baada ya kugongwa na gari au pikipiki wakati wakitoka na kwenda shule.

Amina Said na Wiliamu Kasunzu ambao ni wakazi wa Nyamigota, wanasema kuna baadhi ya familia ambazo zimepoteza watoto kwa sababu ya ajali hizo na baadhi ya watoto wamepata ulemavu kwa kugongwa na gari na pikipiki wakivuka barabara kuu ya kutoka Geita Katoro .

“Kwa kweli tunaipongeza sana serikali kwa ujenzi huu pamoja na kwamba na sisi tumejitolea kuchimba msingi na kusimamia msingi, tunampongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutusaidia ujenzi huu, watoto wetu sasa hawatavuka barabara tena ambako walikuwa wanapoteza maisha” anasema Kasunzu.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, mwalimu mkuu wa shule mama ya msingi Nyamigota Lameck Makesi amesema, ujenzi wa shule hiyo ulianza mwaka jana baada ya serikali kutoa shilingi milioni 240 kwa ajili ujenzi wa vyumba saba vya madarasa.

Kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo mpya pia kumepunguza msongamano wa wanafunzi katika shule jirani za Bwawani, Inyala na Nyamigota na kutembea umbali mrefu kwa wanafunzi wanaotoka kwenye mitaa ya Songambele na Kilimanjaro.

Aidha akizungumza na mwandishi wa blog hii mwalimu mkuu wa shule Mpya ya Jineri Seleman Malingishi amesema, tayari shule hiyo katika kipindi cha mwaka 2024 imewasajili wanafunzi 692 wa darasa la awali na la kwanza.

Malingishi amesema, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,682 na walioandikishwa darasa la kwanza mwaka huu wa 2024 ni wanafunzi 482 huku darasa la awali wakiwa wanafunzi 210.

Diwani wa kata ya Nyamigota Hadija Said amesema, ujenzi huo umekuja baada ya serikali kusikia kilio cha wananchi cha muda mrefu baada ya kuwa zinatokea ajali za mara kwa mara kwa wanafunzi na baadhi ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule.

“Mimi nilipeleka kilio hicho cha wananchi kwenye baraza la madiwani na nilifuatilia hatimaye leo watoto hawavuki barabara tena na hawatembei umbali mrefu kutafuta elimu, ni kweli ajali zilikuwa nyingi, hivyo sasa ni wajibu wa wazazi kupeleka watoto wao kusoma” amesema Hadija.

Post a Comment

0 Comments