MENEJIMENTI ZA HALMASHAURI MKOANI KIGOMA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAPATO




Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amezielekeza Timu za Menejimenti za Halmashauri mkoani hapa kuhakikisha zinasimamia na kudhibi upotevu wa mapato yanayotokana na makusanyo ya ndani katika Halmashauri hizo. 

Mkuu wa Mkoa ametoa  maelekezo hayo alipozungumza kwenye kikao kazi kilichomkutanisha na Timu za Menejimenti za Halmashauri nane za Mkoa wa Kigoma ikiwa ni utekelezaji wa Agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI,  Mohamed Mchengerwa kwa wakuu wa mikoa kukutana na wataalam hao kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kuelekea utekelezaji wa Bajeti 2024/2025 itakayolenga kutatua kero za wananchi.

Amesema ili kudhibiti mapato ya halmashauri, wakurugenzi  wanapaswa kuweka vigezo vya mafanikio kwa wakusanya mapato wa Halmashauri na ambao hawatofikia vigezo hivyo watakuwa wamejikosesha sifa za kuendelea na kazi hiyo. 

Katika hatua nyingine Andengenye amewaelekeza watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Uvinza na Kasulu kuhamia katika Ofisi mpya za wakurugenzi watendaji zilizojengwa katika halmashauri hizo, ifikapo Machi 2024. 

"Serikali imetumia fedha nyingi kutekeleza miradi ya ujenzi wa majengo hayo hivyo nyote mnatakiwa kuhamia na kuanza kuzitumia Ofisi hizo wakati ukamilishwaji wa sehemu zilizobaki ukiendelea" amesisitiza Andengenye.

Kupitia kikao hicho, mkuu wa mkoa ametoa wito kwa wataalam wa Kilimo kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha wanaendelea kutoa kipaumbele katika kilimo cha zao la chikiki ili kuchechemua uchumi wa halmashauri na wananchi kwa ujumla. 

Hata hivyo Andengenye amewakumbusha watumishi wa Umma mkoani hapa kujenga tabia ya kuwekeza katika miradi mbalimbali binafsi  ili kujiimarisha kiuchumi  badala ya kusubiri kutekeleza mipango yao ya kimaendeleo mara baada ya kuhitimisha muda wa  utumishi wa Umma.

Post a Comment

0 Comments