MKOA WA GEITA WAVUKA LENGO LA CHANJO YA SURUA RUBELLA


Na Salum Maige, Geita.

Mkoa wa Geita umefanikiwa kuvuka lengo la chanjo ya surua rubella baada ya kuwapatia chanjo watoto wapatao 584,213 kwenye kipindi cha siku nne za kampeni ya chanjo hiyo kitaifa iliyofanyika kuanzia februari 15 hadi februari 18, mwaka huu wa 2024.

Awali serikali ya mkoa huo iliweka lengo la kuchanja watoto wapatao 517,798 katika wilaya zake tano, lakini kutokana na hamasa na mwitikio wa wazazi na walezi mafanikio hayo yamevuka lengo na kufikia asilimia 112.8.

Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 mkoa wa Geita unakadiriwa kuwa na watoto wapatao 553,228 miongoni mwao wakiwemo watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Akizungumza na mwandishi wa blog hii, Afisa wa chanjo mkoa wa Geita Wille Luhangija amesema,  watoto waliolengwa kupatiwa chanjo hiyo ni wale waliokuwa na umri wa kuanzia miezi tisa hadi miaka mitano.

“Zoezi limeenda vizuri sana  pamoja na hali ya hewa ilikuwa ya mvua,lakini wazazi waliitikia kuleta watoto wao kupata chanjo, tumefanikiwa kwa asilimia kubwa sana hadi tumevuka lengo, lakini pia hamasa kupitia vyombo vya habari na viongozi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji wamehamasisha sana” amesema Luhangija.

Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt.Omary Sukari amesema mkoa huo ulipokea dozi 600,000 za chanjo ya surua rubella kutoka wizara ya Afya kwa ajili ya kampeni hiyo.

“Mafanikio ya kuchanja watoto 584,213 inatokana na uhamasishaji, kila mahali tulipeleka timu na ukiachilia mbali kwenye vituo vya afya tulipeleka hadi kwenye baadhi ya ofisi za serikali za mitaa na vijiji ili kuwapunguzia wananchi kutembea umbali mrefu kufikia huduma hiyo” amesema Dkt Sukari.

Baadhi ya wazazi akiwemo Neema James na Elizaberth Alfredinand ambao ni wakazi wa mjini Geita wameipongeza serikali kuja na kampeni hiyo yenye lengo la kuwalinda watoto wao dhidi ya maradhi yatokanayo na ugonjwa wa surua rubella.


Post a Comment

0 Comments