MUME AMUUA MKE WAKE KWA KUMNYONGA KISHA NAE KUJINYONGA MKOANI KIGOMA


Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
RASHIDI Mkayala mkazi wa mtaa gemu kata ya Mwanga Kusini Manispaa ya Kigoma Ujiji amemuua mke wake Bernadeta Cosmas(33) kwa kumnyonga shingo hadi kufa chanzo kikielezwa kuwa ni  mgogoro baina ya wanandoa hao.

Muda mfupi baada ya Mkayala kutekeleza tukio la kumnyonga mkewe, naye alijinyonga kwa kutumia kilemba cha kiume cha kuvaa kichwani.

Akielezea chanzo cha tukio hilo lililotokea usiku wa kuamakia leo tarehe 21 February 2024, mwenyekiti wa mtaa wa gemu, Buswalu Mkama amesema chanzo ni mgogoro uliotokea siku za nyuma ambapo mke wa marehemu alifika kwa mwenyekiti huyo na kutoa taarifa ya vitendo vya  mume wake kuuza vitu vya ndani bila makubaliano baina yao.

Amesema amekuwa akisuluhisha kesi za wanandoa hao ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika ofisi yake mara kadhaa kwaajili ya kutafutiwa ufumbuzi na kuondoa changamoto.

“Siku moja kabla tukio Bernadetha alilala nyumbani kwangu baada ya kumkimbia mumewe  kutokana na kipigo alichokipata, alinusurika kuuawaa kwa kunyongwa na waya wa umeme,  alipopata nafasi ya kuchomoka alikimbilia kwangu  ambapo alilala na kuondoka kesho yake (siku ya tukio)” ameeleza mwenyekiti

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa marehemu Hussein alimnyonga mkewe kwa mikono hadi kumuua na baadaye kutoka nje ambapo alifunga mlango kwa nje na kurudi ndani kwa kupitia dirishani ambapo alifunga milango yote na madirisha na yeye kujinyonga  kwa kitambaa cha kichwani.

Kwa upande wa mtoto wa marehemu, Hussein Rashidi amesema wazazi wake wamekuwa wakigombana mara kwa mara  na kwamba mama yake alikuwa akimkimbia baba yake na kulala kwa viongozi wa serikali za mitaa ili kujinusuru asiumizwe kutokana na vipigo alivyokuwa akipata kutoka kwa baba yake.

Hadi sasa  miili ya wanandoa hao imehifadhiwa kwenye hospitali ya mkoa ya rufaa ya Maweni wakati jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments