TAMISEMI YATOA MAGARI 7 KWAAJILI YA USIMAMIZI SHIRIKISHI SEKTA YA AFYA KIGOMA


Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amekabidhi magari Saba yaliyotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Wizara ya Afya kwa ajili ya kufanya usimamizi Shirikishi wa utoaji Huduma  katika Sekta ya Afya kwa Mkoa wa Kigoma. 

Akizungumza kabla ya kukabidhi magari hayo, Andengenye amesema awali mkoa ulishapokea magari nane kwa ajili ya kubeba wagonjwa kutoka OR-TAMISEMI hivyo kupokelewa kwa magari hayo kumeongeza idadi na kufikisha jumla ya magari 15,  jambo litakaloongeza  ufanisi katika utendaji  kazi wa sekta hiyo.

Aidha, Andengenye amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya mkoani Kigoma ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Afya, upatikanaji wa vifaa tiba na dawa sambamba na kuendelea kuwawezesha watendaji nyenzo za usafiri ili waweze kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za kuaminika katika Hospitali, vituo vya Afya na Zahanati. 

"Nichukue fursa hii kuwataka watakauhusika na matumizi ya magari haya kuzingatia malengo yaliyokusudiwa sambamba na kuyawekea utaratibu wa matengenezo utakaozingatia wakati sahihi sambamba na kuwakabidhi madereva wenye weledi ili yaweze kudumu na kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu" amesisitiza Andengenye. 

Magari hayo yamegawiwa katika vitengo vya usimamizi Sekta ya Afya katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Chuo cha Afya cha Matibabu Maweni, pampja na Halmashauri ya Mji Kasulu na Wilaya za Kibondo,  Uvinza na Buhigwe.

Post a Comment

0 Comments