TANZANIA, CONGO DR ZAWEKA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA MAJANGA


Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Kamati za Maafa Mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa ya Kivu Kusini na Tanganyika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimekutana ili kubadilishana mbinu, kujadili na kuweka mikakati ya pamoja yenye lengo la kukabiliana na majanga katika ukanda huo. 

Akifungua Mkutano uliozikutanisha Kamati hizo na kufanyika mkoani humo Februari 20-21 2024, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema athari za majanga huwa hazina mipaka ya kijiographia hivyo ni jambo jema kwa pande hizo kuweka mikakati ya pamoja ili kuepusha au kupunguza madhara kwa wakazi. 

Ameyataja majanga ambayo yamekuwa yakiendelea kuleta athari katika ukanda huo kuwa ni ukosefu wa amani,  magonjwa ya mlipuko, ongezeko la wakimbizi, uharibifu wa Mazingira, mafuriko, kuongezeka kwa kina cha Maji  Ziwa Tanganyika pamoja na ajali za mara kwa mara katika ziwa hilo. 

Kupitia kikao hicho, Mkuu huyo wa mkoa amezitaka kamati hizo  kuweka mikakati ya kudumu katika kushughulikia majanga mbalimbali yanayojitokeza ili kupunguza athari zake ikiwemo vifo, ukosefu wa amani, uharibifu wa mazingira na mdororo wa kiuchumi. 

Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la REDESO mkoa wa Kigoma Emmanuel Solomon amesema kamati zinakabiliwa na changamoto za udhaifu kwenye usimamizi wa Sheria na Miongozo inayotungwa na serikali katika nchi hizo mbili. 

Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni ongezeko la wahamiaji haramu kutoka Congo kuingia Tanzania, ufinyu wa bajeti kwa ajili ya kuziwezesha kamati kufanya ufuatiliaji sambamba na uelewa mdogo wa wakazi wa maeneo hayo kuhusu athari za majanga ili kushiriki kuchukua tahadhari. 

Akitaja mapendekezo ya pamoja ya kikao hicho, Solomon amesema Serikali za pande zote mbili zinapaswa kutilia mkazo katika kusimamia utendaji kazi wa kamati sambamba na kuziwezesha kifedha ili zimudu kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.

Post a Comment

0 Comments