WANAOPISHA UWANJA WA NDEGE KIGOMA WAMLILIA RAISI SAMIA

Baadhi ya nyumba za kata ya Kitongoni Manispaa ya Kigoma Ujiji ambazo zitavunjwa na kulipwa fidia kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma.


Salama Bilali mmoja wa wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ambaye nyumba yake inavunjwa na kulipwa fidia kupisha mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege kigoma.

Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAKAZI 360 kutoka kata tatu za manispaa za manispaa ya Kigoma Ujiji ambao nyumba zao zitavunjwa kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma wamepiga goti na kumuomba Raisi Samia Suluhu Hassan kuingilia kati kuiwezesha  serikali kuharakisha kulipa fidia ya maeneo kutokana na adha kubwa wanayopata sasa baada ya kuzuiwa kutofanya chochote kwenye maeneo hayo.
 
Wakizungumza na waandishi wa Habari mjini Kigoma wananchi hao walisema kuwa mwaka mmoja sasa tangu walipopewa notisi ya kutofanya chochote kwenye maeneo hayo baada ya uthamini kufanyika lakini hali wanayokumbana  nayo sasa inatia simanzi kubwa.
 
Mmoja wa wananchi hao, Fadhili Hamisi Mayogela kutoka kata ya Machinjioni Ujiji mjini Kigoma alisema kuwa tangu mwezi Machi mwaka jana walizuiwa kutofanya chochote kwenye nyumba hizo kwa maelekezo kwamba  watalipwa fidia ya maeneo yao ndani ya miezi sita lakini hakuna kilichofanyika.
 
Kufuatia hali hiyo mwananchi mwingine Salama Ramadhani Bilali  amemuomba Raisi Samia Suluhu Hassan aingilie kati suala hilo kutokana na sintofahamu inayokumba na kwamba kama serikali haina pesa za kulipa kwa sasa iwaruhusu wafanyie ukarabati nyumba zao na fidia ifanyike serikali itakapopata fedha za kulipa.

Akizungumzia hali hiyo Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye amekiri kuwepo kwa mpango wa fidia kwa wananchi wa kata tatu za manispaa ya Kigoma Ujiji ambao wanapaswa kuondoka maeneo yao kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma.
 
Mkuu huyo wa mkoa amekiri kuchelewa kufanyika kwa malipo hayo ingawa amebainisha kwamba serikali inafanya juhudi kuhakikisha malipo hayo yanafanyika ili malipo ya fidia yasiwe kikwazo kwa utekelezaji wa mradi huo.

Post a Comment

0 Comments