Na
Mwandishi Wetu, Kenya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kazi ya uchorongaji wa visima vya Jotoardhi nchini Tanzania itaanza mwezi Aprili mwaka huu ili kuweza kuhakiki rasilimali ya Jotoardhi iliyopo kabla ya kuanza kwa shughuli za uzalishaji umeme kutokana na nishati hiyo.
Dkt. Biteko amesema baada ya kutembelea vyanzo na mitambo ya kuzalisha umeme wa Jotoardhi katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya.
“Tumekuja kwenye mitambo ya kuzalisha umeme unaotokana na Jotoardhi inayomilikiwa
na kampuni ya uzalishaji umeme ya Kenya (KenGen) na tumejionea jinsi
walivyopiga hatua kwenye uendelezaji wa rasilimali hii kwani tayari wanazalisha
umeme wa Jotoardhi wa kiasi cha megawati zaidi ya 799.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema Tanzania kwa upande wake, tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya
kuendeleza vyanzo vya Jotoardhi na kwamba kampuni ya KenGen mwezi Aprili mwaka
huu itakuwa mkoani Mbeya kwa ajili ya kuanza uchorongaji vyanzo vya Jotoardhi
katika eneo la Ngozi na Kiejo-Mbaka kwa kushirikiana na kampuni ya Uendelezaji
wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).
Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya KenGen ya Kenya kwa hatua kubwa waliyofikia katika uendelezaji wa Jotoardhi ambapo zaidi ya asilimia 60 ya umeme nchini humo unatokana na nishati hiyo.
Ametanabaisha kuwa, Tanzania imeamua kuongeza vyanzo vya uzalishaji umeme na sasa nguvu kubwa inawekwa kwenye kuendeleza miradi kama hiyo ya Jotoardhi ili kupata umeme wa kutosha kwa ajii ya wananchi.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Maendeleo ya Jotoardhi katika kampuni ya
KenGen, Peketsa Mangi amesema kuwa, nchi hiyo imekuwa na ushirikiano mzuri na
Tanzania katika kuhakikisha nchi hizo zinafanikiwa katika uendelezaji wa
Jotoardhi.
Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia nafasi KenGen kufanya kazi kwa
pamoja na wataalan kutoka TGDC ili kuchimba visima vya uhakiki wa rasilimali
hiyo nchini na kueleza kuwa, kampuni hiyo ipo tayari kufanya kazi husika kwa
mafanikio.
Viongozi walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwenye ziara
hiyo ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba,
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Benard Kibesse na Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.
0 Comments