GEITA YATAJA MAENEO HATARISHI YA MAAMBUKIZI YA KIFUA KIKUU


Na Salum Maige, Geita.

Zikiwa zimebaki siku chache Tanzania kuungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya ugonjwa wa kifua kikuu duniani mkoani Geita maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu,uvuvi na shuleni yametajwa kuwa maeneo hatarishi yanayosababisha maambukizi ya ugonjwa huo kwa wananchi.

Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani hufanyika siku ya machi 24, ya kila mwaka ambapo katika mkoa wa Geita maadhimisho hayo yatafanyika kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe eneo ambalo hufanyika shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Kwa mujibu wa takwimu za idara ya afya kitengo cha kifua kikuu hospitali ya rufaa mkoa wa Geita ni kwamba mwaka jana 2023 lengo ilikuwa ni kuibua wagonjwa 4,422  lakini waliopatikana ni 3,937 sawa na asilimia 89.

Pia, takwimu hizo zinaonyesha kuwa katika kipindi hicho cha mwaka 2023 watoto walioibuliwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu ni watoto 485 sawa na asilimia 13 pungufu ya malengo ya asilimia 15.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa niaba ya mratibu wa kifua kikuu mkoa wa Geita, Dkt Protas Manyerezi amesema maeneo hayo yamekuwa na kasi ya maambukizi kutokana na mikusanyiko ya watu wengi wanaovutiwa madini na samaki.

Dkt.Manyerezi amefafanua kuwa, kwa upande wa shule kumekuwa na mikusanyiko ya wanafunzi na kwamba baadhi yao waliopimwa wamegundulika kuwa na ugonjwa huo, na hivyo kushauri madarasa na mabweni kujengwa na kuacha nafasi kubwa za kupitisha hewa.

“Ugonjwa wa kifua kikuu huambukizwa kwa njia ya hewa, hivyo sisi kama mkoa tunapita kwenye maeneo yenye mikusanyiko kama hayo kuwapa elimu wananchi na kuwapima ili kuwabaini wenye shida na kuwaanzishia matibabu ambayo hutolewa bure”, anasema Dkt.Manyerezi.

Aidha, amesema wanaume wengi ndiyo wamegundulika kuwa na maambukizi zaidi ya kifua kikuu ikilinganisha na wanawake kutokana na mazingira ya kazi wanazofanya wanaume tofauti na wananwake.

“mfano ukienda kwenye shughuli za uvuvi na machimbo wengi wanaojishughulisha na maeneo hayo ni wanaume tofauti na wanawake,hivyo tumekuwa tukipata wanaume wengi zaidi kuliko wanawake” anasema Dk.Manyerezi.

Post a Comment

0 Comments