RC ANDENGENYE AKABIDHI MSAADA YA ZAIDI YA TSH. MIL 25 KWA WAHANGA WA MAAFA KAKONKO.





Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amekabidhi msaada wa Chakula pamoja na mabati wenye thamani ya zaidi ya  Shilingi Mil. 25 kwa  wahanga wa maafa yaliyotokana na mvua kali zilizonyesha katika kipindi cha Mwezi Januari 2024 wilayani Kakonko.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo uliojumuisha mabati 1,000 na mahindi  tani tano (5), Andegenye amesema serikali itaendelea kuwagusa wahanga hao kupitia misaada mbalimbali  ili kuwapunguzia adha iliyosabaishwa na maafa hayo. 

Aidha Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa mashirika ya Umma na binafsi kujitokeza  na kutoa misaada mbalimbali kwa wahitaji  hao kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali za kuwathamini wananchi wake.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amesema kupitia msaada huo ulioidhinishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, wilaya ilipokea kilo 5,184 za mahindi pamoja na Shilingi Mil. 25 kwa ajili ya kufanya manunuzi ya mabati 1,000.

Ameeleza kuwa msaada huo utagawiwa kwa jumla ya wanakaya 216 katika vijiji vya Kakonko, Mbizi, Itumbiko, Kanyonza, Cholambo, Kiga na Nyagwijima ambapo kila kaya itapatiwa bati 20 na kila  mwanakaya atapatiwa kilo 24 za mahindi. 

"Niishukuru serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais. Dkt. Samia Suluhu kwa kuguswa na kuonesha kuthamini wananchi hususani wenzetu waliopatwa na maafa  ndani na nje ya halmashauri yetu ya Kakonko" amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya. 

Mvua hizo zilizoambatana na upepo mkali zilisababisha vifo vya watu wawili (2), majeruhi,  uharibifu wa nyumba 47 na kusababisha  jumla ya watu 216 kukosa makazi.

Post a Comment

0 Comments