SHUGHULI ZA KIBINADAMU CHANZO CHA KUONGEZEKA KINA CHA MAJI ZIWA TANGANYIKA



Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Shughuli za kibinadamu na uwepo wa Majanga ya asili vimetajwa kuwa ni sababu ya kuongezeka kwa kina cha Maji katika Ziwa Tanganyika. 

Hayo yamebainishwa kupitia Mkutano wa Mwaka wa Kamati za kukabiliana na Majanga katika mkoa wa Kigoma na mikoa jirani ya nchi ya Burundi uliofanyika katika Ukumbi wa NSSF Manispaa ya Kigoma Ujiji mjini Kigoma. 

Imebainishwa kuwa  tafiti zilizofanywa zimeonesha, athari za majanga ya asili ikiwemo milipuko ya Volkano katika baadhi ya milima nchini Congo DR, husababisha lava iliyopoa pamoja na udongo  kuingia katika mto Lukuga  kisha kuzuia  maji kupita kwa ufanisi na kuingia katika bahari ya Atlantic. 

Kupitia kikao hicho, imebaika kuwa  ongezeko la shughuli za kibinadamu pembezoni mwa mto Lukuga zinasababisha mmomonyoko wa ardhi hivyo mchanga hujaa katika mto huo na kutoruhusu maji kupita kwa  ufanisi  kutoka ziwa Tanganyika ili kuingia baharini. 

Baadhi ya athari za ongezeko la kina cha maji katika Ziwa Tanganyika  ni maji  kujaa katika maeneo yaliyojengwa miundombinu mbalimbali hususani bandari na makazi, kupotea kwa fukwe pamoja na baadhi ya mito inayoingiza maji ziwani humo kufurika na kuathiri mashamba na makazi.

Aidha ongezeko la maji katika ziwa Tanganyika,  uhamiaji holela wa wakazi ili kutafuta usalama au fursa za kimaisha, milipuko ya magonjwa pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira vimetajwa kuwa ni sehemu ya majanga katika mkoa wa Kigoma na mikoa jirani ya nchi za Burundi na Congo DR kupitia mkutano huo.

Post a Comment

0 Comments