WAKIMBIZI KUTOKA BURUNDI WAHAMASISHWA KUREJEA NCHINI MWAO


Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
Zaidi ya wakimbizi laki moja kutoka nchini Burundi wanaopatiwa hifadhi katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma wametakiwa kurejea nchini mwao kwa hiyari kupitia mpango wa hamasa unaotarajiwa kufikia tamati Desemba 31, 2024. 
-
Akizungumza kwa nyakati tofauti na  wakimbizi wa nchi hiyo  waliopo katika Kambi za Nduta na Nyarugusu mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema mara baada ya kukamilika kwa mpango huo wakimbizi hao watapoteza hadhi ya ukimbizi nchini. 
-
Amesema Mpango unalengo la kuhakikisha kila mkimbizi kutoka Burundi anarejea kwa amani, utu na Utulivu kwani kwa sasa nchi hiyo ina usalama na amani hivyo wanapaswa kujitoa katika maisha ya ukimbizi na kwenda kuimarisha uchumi wa Taifa lao. 
-
Andengenye amesema kupitia mpango huo kila mkimbizi atakayerejea nchini humo atapata dola mia mbili (200) za kimarekani, mgao wa chakula kwa muda wa miezi mitatu sambamba na familia kuondoka na mabati kwa ajili ya kwenda kuanza ujenzi. 
-
"Mpango huu wa hamasa ulianza Januari Mosi, 2024, na unatarajiwa kufikia tamati Desemba 31, 2024 ambapo  mashirika yote yanayotoa misaada kwa wakimbizi yatasitisha huduma kufuatia mikataba yao kufikia tamati, hivyo niwasihi mtumie fursa hii itakayowafanya  mrudi nchini mwenu kwa hadhi na heshima" amesisitiza Andengenye. 
-
Mratibu wa Idara ya wakimbizi mkoa wa Kigoma Mwita  Chacha amewakumbusha wakimbizi hao kutumia muda wa miezi nane uliobaki kuondoka nchini kutokana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) kujielekeza kutoa huduma katika maeneo yenye uhitaji mkubwa hususani yenye machafuko na ukosefu wa amani. 
-
"Nchi ya Burundi kwa sasa ina amani hivyo mashirika ya Umoja wa mataifa yanayotoa huduma kwenu  yanaelekeza usaidizi wake kwenye  maeneo yenye hali ya ukosefu wa amani kutokana na vita kama Ukraine,  Congo DR, Sudani na eneo la Mashariki ya kati" amefafanua Chacha. 
-
Jumla ya wakimbizi na waomba hifadhi 48, 099 kutoka nchini Burundi wanahifadhiwa katika Kambi ya wakimbizi Nyarugusu wilayani  Kasulu  huku wengine 64,588 wakipata hifadhi  katika kambi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo.

Post a Comment

0 Comments