WAKRISTU KIGOMA WAMETAKIWA KUISHI MAISHA YA UTAKATIFU





Na Diana Rubanguka, Kigoma.
Waumini wa Kanisa Katoriki mkoani Kigoma wametakiwa kuishi maisha ya utakatifu  na kuifanya kazi ya Mungu kwa ukamilifu ikiwemo kuwasaidia watu wasiojiweza.

Wito huo umetolewa na Makamu Askofu Jimbo Katoriki Kigoma, Padre Evaristi Guzuye wakati wa hitimisho la maandamano ya  ibada ya  njia ya msalaba iliyofanyika kuanzia Parokia ya Mtakatifu Vicenti wa Paulo Katubuka hadi kituo cha Hija Buhabugali kilichopo eneo la Katonga Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Padre Guzuye amesema, siku ya ijumaa kuu ni siku ambayo waamini wote wa kanisa Katoriki Duniani wanaadhimisha siku ya kumbukumbu ya kifo cha Bwana Yesu Kristu, kifo ambacho kinaambatana na mateso makali hivyo kutokana na ibada ya leo waamini wote wanaaswa kutokata tamaa kwa kubeba mahangaiko ya wengine hasa wahitaji, ikiwa ni kuuenzi upendo walioachiwa na Yesu.

"Siku ya leo tunaadhimisha ijumaa kuu, siku ya ijumaa kuu ni siku ambayo bwana wetu Yesu Kristu alikufa kifo cha juu ya msalaba kwa mateso makali mno, ni siku ambayo dunia nzima waamini wote wa kanisa katoriki tunakusanyika kwa ajili kukumbuka kifo hicho na ujumbe wa leo ni kwamba kwa Kifo hiki kinatukumbusha kuwa Bwana Yesu alitupenda, na aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu" amesema Padre Guzuye.

Akizungumza katika maandano hayo ya njia ya msalaba Paroko Msaidizi Parokia ya Bikira Maria  Mshindaji Kigoma Padri George  Ntomoka amesema, lengo la kuandamana ni kutaka waamini wapate muda mrefu wa kusali huku wakiyatafakari mateso ya Bwana Yesu Kristu.

"Waamini wapate muda mrefu wa kuyatafakari mateso ya Bwana wetu Yesu kristu hali kadhalika sababu ya kuhitimisha katika kitu hiki cha hija cha Jimbo ni, maandano haya ni sehemu ya hija hivyo waamini wamepata fulsa ya kushiriki hija kwa ijumaa kuu hii ya mwaka 2024" Ameeleza Padre Ntomoka.

Kwa mujibu wa Padre Ntomoka, Kifo cha Bwana Yesu Kristo ndiyo kiini cha imani ya wakristu, kwani Yesu aliteswa akafa na akafufuka ambalo ndilo fumbo la wokovu wa wakristu hivyo wakristo wanapaswa kujifunza kwamba mateso na kifo chake vinapaswa kuimalisha imani ya wakristu wa Katoriki.

Kwa niaba ya kamati ya maandalizi Katekista kigango cha Katubuka Scholastica John amesema wiki kuu ni wiki ambayo imebeba azimisho kubwa la siku 40 za mfungo wa kwaresma, wiki kuu imebeba hitimisho la kazi ya Yesu Msalabani.

Kupitia wiki hii wakristu wote hasa wakatoriki wanapaswa kuyaishi maisha ya Bwana Yesu kwa kuuenzi upendo anaoufanya juu ya watu wake na kuyaishi maagizo yaliyotolewa na Yesu kwa kutambua kazi aliyoifanya msalabani.


Post a Comment

0 Comments