BAJAJI, BODA BODA WASEMA WAKO TAYARI KULIPA KODI KWA HIARI




Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Waendesha pikipiki (bodaboda) na bajaji mkoani Kigoma wamesema kuwa wako tayari kulipa kodi ya mapato kwa hiari kutokana na biashara ya usafirishaji wanayofanya wakiunga mkono mabadiliko ya sheria ya kodi iliyopitishwa na serikali mwaka 2023.
 
Waendesha bajaji hao na boda boda wametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa pamoja baina yao na maafisa wa Mamlaka ya mapato (TRA) mkoa Kigoma mkutano uliokuwa ukitoa elimu na ufafanuzi wa sheria hiyo kwa waendesha pikipiki hao.
 
Mwenyekiti wa waendesha boda boda mkoa Kigoma, Samwel Mtema akizungumza katika mkutano huo alisema kuwa wamesikia uwepo wa mabadiliko ya sheria hiyo ya kodi iliyopitishwa na bunge na kwamba hawana pingamizi katika utekelezaji wa sheria hiyo.
 
Kwa upande wake Mussa Edson Mwenyekiti wa kijiwe cha boda boda Nazareth Manispaa ya Kigoma Ujiji 
 alisema kuwa mkoa Kigoma umepiga hatua kubwa kwenye maendeleo ukiwemo ujenzi wa miundo mbinu ya barabara za lami ambayo msingi wake ni kodi inayokusanywa hivyo kwa upande wao wamelipokea hilo ili kuunga mkono serikali katika ukusanyaji wa mapato yatakayogharamia shughuli za maendeleo ikiwemo kodi ya shilingi 65,000 wanayotakiwa kulipa kwa mwaka.
 
Akifungua mkutano huo Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kali amewataka waendesha pikipiki na bajaji kulichukulia suala la kulipa kodi kwa umakini kutokana na serikali kujali uwepo wao kama wafanyabiashara lakini pia kama sehemu inayotoa ajira kubwa kwa watanzania.
 
Akizungumza katika mkutano huo Msimamizi Msaidizi wa kodi kutoka idara ya elimu kwa mlipa kodi na mawasiliano TRA mkoa Kigoma, Makilo Seuta alisema kuwa mkutano huo unalenga kutoa elimu na ufafanuzi kwa waendesha pikipiki hao na bajaji wakati utaratibu wa kundi hilo kuanza kulipa kodi utakapoanza.

Makilo alisema kuwa kodi hiyo ni sehemu ya mabadiliko ya Sheria za kodi ya mwaka 2023 ambapo serikali imeweka kodi ya mapato kwa wasafirishaji wa abiria kwa kutumia pikipiki zenye magurudumu mawili (Bodaboda) ambao watatakiwa kulipa kiasi cha Sh. 65,000 kwa Mwaka.
 

Post a Comment

0 Comments