MGAO WA MAJI KUONDOLEWA KIGOMA UJIJI - KUWASA

Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA Poas Kilangi akizungumza kwenye mkutano na viongozi wa serikali za mitaa na watumishi wa KUWASA (KUWASA DAY)
Mkuu wa wilaya Kigoma Salum Kali (kulia) akikabidhi funguo ya moja ya pikipiki tano kwa fundi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kigoma Ujiji.


Na Fadhili Abdallah, Kigoma
Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira  Kigoma Ujiji (KUWASA) imesema kuwa imejipanga kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana kwa saa 24 kwa wakazi wa manispaa ya Kigoma Ujiji lengo ikiwa ni kuhakikisha kila mkazi wa mji huo anapata  maji muda wote.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA, Poas Kilangi alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya utendaji ya mamlaka hiyo kwa viongozi wa serikali za mitaa na watumishi wa mamlaka hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki tano kwa watendaji wa mamlaka hiyo na kuwapongeza watendaji waliofanya vizuri.
 
Kilangi alisema kuwa wakati huu ambapo mradi mkubwa wa maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 42 ukiwa umekamilika wanapambana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha upatikanaji maji kwa wananchi ikiwemo mivujo inayotokana na kuchakaa kwa baadhi ya miundo mbinu ya kupeleka maji kwa wananchi ambayo kwa sasa wako kwenye hatua ya utekelezaji kuondoa changamoto hiyo.
 
Akielezea  kukabidhiwa kwa pikipiki tano kwa watendaji wa mamla hiyo zilizotokana na mapato ya ndani alisema kuwa itatimiza azma yao ya kufanya kazi saa 24 hasa watumishi wa idara ya ufundi na miundo mbinu ili kushughulikia tatizo la upatikanaji maji wakati wote bila watendaji hao kuathiriwa na changamoto ya usafiri kufika maeneo ya kazi.
 
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kali alisema kuwa serikali imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha inapeleka huduma kwa wananchi wake ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama Kigoma Ujiji hivyo kuwataka viongozi hao wa serikali za mitaa kusaidia mamlaka katika kutoa taarifa za mivujo ya maji inapotokea.
 
Akizungumzia kukabidhiwa kwa vitendea kazi hivyo Mkuu huyo wa wilaya  alisema kuwa ni sehemu ya mpango wa serikali katika kurahisisha utendaji na kuwataka watumishi waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitumia kulingana na malengo na mpango wa mamlaka ili kufanikisha utoaji huduma kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments