RC ANDENGENYE: UMOJA, AMANI NA MSHIKAMANO, MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA












Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mh. Thobias Andengenye amesema maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa na kuwanufaisha watanzania  yametokana na msingi wa Umoja, Amani na Mshikamano uliojengwa na waasisi wa Taifa la Tanzania. 

Akizungumza na wakazi wa mkoa wa Kigoma waliojitokeza kwenye kilele cha Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya mjini Kasulu, Andengenye amesema kuimarika kwa uchumi wa nchi sambamba na uboreshwaji mkubwa wa mazingira ya utoaji huduma kwa jamii ni matokeo ya kudumisha tunu za Taifa  ikiwemo Muungano.

"Wanakigoma wanashuhudia upatikanaji wa uhakika wa huduma za Maji, Umeme, maboresho ya miundombinu ya kitaaluma, upatikanaji huduma bora  za Afya sambamba na uboreshwaji mkubwa wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji yote yakiwa ni matunda ya Muungano" amesema Andengenye. 

Kupitua hotuba yake Andengenye amewakumbusha wakazi mkoani hapa na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuulinda muungano na kuudumisha ili kuliweka taifa katika hali ya amani na utukivu, jambo litakalotoa fursa kwa wananchi kuelekeza nguvu na akili zao katika uzalishaji mali na kuinua uchumi wa Taifa. 

"Tumeendelea kushuhudia amani na utulivu chini ya Muungano wetu huku sote tukiwa mashahidi kuhusu namna ambavyo serikali zote mbili zimekuwa zikijiendesha kwa uwazi chini ya misingi ya kidemokrasia, kuzingatia utawala bora pamoja na  sheria" amesema Andengenye.

Aidha Andengenye amehitimisha kwa kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu pamoja na Dkt. Hussein Mwingyi Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuudumisha muungano na kuwaletea Maendeleo wananchi.

Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa mkoa wa Kigoma yamefanyika katika Uwanja wa Umoja Halmashauri ya Mji Kasulu yakihudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Mhe. Hassan Rugwa, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini Dkt. Joyce Ndalichako, Kamati ya Usalama Mkoa, wakuu wa wilaya, makatibu Tawala wa wilaya, wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za Mitaa, wakuu wa Taasisi za Umma, Viongozi wa vyama vya Siasa pamoja na viongozi wa dini.

Post a Comment

0 Comments