MADAKTARI BINGWA 60 KUPIGA KAMBI KIGOMA


Mkuu wa mkoa Kigoma akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa kambi ya kanda ya madaktari bingwa mkoani Kigoma.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni Dk.Stanley Binagi.

Lango kuu la kuingia hospitali ya mkoa Kigoma Maweni.

Na Fadhili Abdallah, Kigoma
Mkuu wa mkoa Kigoma amewaita wananchi wa mkoa huo katika hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni kupata huduma za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ambao watapiga kambi hospitalini hapo kwa siku tano.

Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye akizungumza na waandishi wa Habari mjini Kigoma alisema
kuwa madaktari  bingwa 60 kutoka mikoa ya Kigoma,Tabora,Katavi na Rukwa wanatarajia kupiga kambi kwa siku tano mkoani Kigoma  kuanzia Mei 6 hadi 10 mwaka huu ikiwa ni mwendelezo wa kambi za Matibabu zinazofanyika mikoa mbalimbali nchini maarufu kambi ya matibabu ya Raisi Samia.

Mkuu huyo wa mkoa Kigoma ametoa wito kwa wananchi wa mkoa Kigoma kujitokeza kwa wingi ili  kupima afya na kupata matibabu yakiwemo ya kibingwa na kwamba zitafanyika pia operesheni ambazo hazikuwa zinafanyika kwenye hospitali ya mkoa Kigoma Maweni kutokana na ukosefu wa madaktari bingwa wa fani hizo.
 
Andengenye Mkuu  alisema kuwa kufanyika kwa kambi hiyo ni sehemu ya mpango wa serikali chini ya Raisi Samia Suluhu Hassan kusogeza huduma za matibabu hasa ya Kibingwa ambayo watu wengi wanahitaji lakini hawapati fursa ya kuyapata kutokana na kutokuwepo kwa mabingwa wa fani hizo na kushindwa  gharama ya kufuata huduma hizo nje ya mkoa.
 
Akizungumzia kufanyika kwa kambi hiyo Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa Kigoma Maweni, Dk.Stanley Binagi alisema kuwa kwa muda wa siku tano ambazo huduma hiyo itakuwa inatolewa wagonjwa Zaidi ya 3000 wanatarajia kuonwa na madaktari hao.
 
Dk.Binagi alisema kuwa kufanyika kwa kambi hiyo inayofanyika kikanda ni msaada mkubwa kwa watu wa mkoa Kigoma ambao walikuwa wakihitaji huduma za kibingwa lakini walizikosa ndani ya mkoa kwa kutokuwepo kwa madaktari bingwa wa magonjwa yao lakini walishindwa kusafiri kufuata huduma hizo nje ya mkoa kutokana na hali mbaya ya kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments