WAKULIMA WADOGO WAFUNDWA KUFANYA KILIMO BIASHARA






Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mafunzo yanatolewa kwa wakulima  125,000 kutoka mikoa ya Kigoma na Kagera  kupata elimu ya kilimo bora ili kutekeleza mpango wa kilimo chenye tija na kukifanya kilimo kuwa biashara ambayo itabadilisha uchumi wa wakulima hao.
 
Meneja mradi kutoka Shirika la Nyakitonto Youth Development, Elvas Mbogo alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa wakulima wawezeshaji kutoka halmashauri tano za mkoa Kigoma ambao wanapewa elimu ili kufikisha elimu hiyo kwa wakulima wadogo vijijini.
 
Mbogo alisema kuwa mafunzo hayo yanayofadhiliwa na TAASISI ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) yanalenga kuwafanya wakulima hao kulima kwa kufuata ushauri waa kitaalam kuanzia kuandaa mashamba, usimamizi wa shamba, matumizi ya pembejeo na utafutaji wa masoko kwa ajiili uhakika wa soko la mazao hayo.
 
Kwa upande wake Afisa uwezeshaji vijana na wanawake, Mnyoroka Kilio alisema kuwa Pamoja na lengo kuu la mradi huo la kuwapa elimu wakulima wadogo kulima kitaalam na kuongeza uzalishaji ili kilimo kukifanya kuwa biashara kubwa lakini pia mradi huo unalenga kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana kwenye sekta ya kilimo.
 
Akifungua mafunzo hayo Mhandisi wa umwagiliaji kutoka sekreatariet ya mkoa Kigoma, Bathoromeo Morris alisema kuwa mafunzo hayo kwao katika sekta ya uchumi na uzalishaji ni muhimu kwani inaunga mkono mkakati wa serikali ya mkoa katika kuwapa wakulima utaalam ambao utasaidia kuongeza uzalishaji.
 
Morris alisema kuwa kutolewa elimu kwa wakulima hao kunawapa nafasi ya kuwa na takwimu ya kupanga mipango ya baadaye ya kilimo chenye tija kuwatumia wakulima hao ambao wanakuwa wamepata elimu ya kilimo cha kisasa na elimu ya kilimo biashara.

Post a Comment

0 Comments