WAVUVI KIGOMA WALALAMIKIWA KWA KUJIHUSISHA NA MAPENZI DHIDI YA WANAFUNZI





Na Kadislausi Ezekiel, Kigoma
WAVUVI katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma, wamelalamikiwa na wananchi pamoja na wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, kwa kujihusisha na mapenzi dhidi ya Wanafunzi, na kupelekea watoto wengi wa kike kushidwa kutimiza ndoto zao.
 
Wakazi  katika Kijiji cha Kigalye kata ya Ziwani, wameibua hoja hiyo kuhusu watoto wa kike kukatiza masomo kwa kupewa mimba na baadhi ya wavuvi wasiokuwa waadilifu kwenye kikao cha wazazi, wadau wa uvuvi na viongozi kilichoandaliwa na Shirika la FAO Chini ya Mradi wa FISH 4ACP, kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Sokoine kampasi ya Mizengopinda Katavi.

Wazazi hao akiwemo Issaya Enos na Mkuu wa shule ya Sekondari Ziwani Raymond Liberati, wameomba hatua zichukuliwe kwa wanaokwamisha ndoto za wanafunzi, pamoja na kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake. 
 
Aidha Viongozi mbalimbali akiwemo mtafiti na mshauri wa masuala ya maendeleo kutoka chuo kikuu cha Sokoine SUA kampasi ya Mizengopinda Katavi, Profesa Anna Sikira amesema, wamelazimika kuandaa mkutano huo  pamoja na Viongozi ili kusaidia kupunguza ukatili wa kijinsia, uongozi na kuwezesha wanawake kushiriki katika masuala ya Uvuvi.
 
Pamoja na hayo, Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya kigoma Yassin Tenganya, licha ya kukiri uwepo wa mimba za utotoni kwa wanafunzi, amesema hatua zinadhidi kuchukuliwa kwa wahusika, na kuitaka jamii kutofumbia macho vitendo hivyo vya ukatili.

Aidha mafunzo hayo pia, yameenda sambamba na masuala ya uongozi na ufugaji wa mazao ya uvuvi hasa Samaki, ambapo wadau wa uvuvi katika ziwa Tanganyika wamenufaika nayo ili kuhakikisha mnyororo wa thamani wa uvuvi unaimarika.
 

Post a Comment

0 Comments